Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Waziri wa Barabara na Maendeleo ya Miji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Farzaneh Sadegh, amesema kuwa miradi ya ujenzi wa barabara na makazi iliendelea kutekelezwa licha ya changamoto zilizotokana na kile alichokiita vita vilivyolazimishwa vya tatu.
Akizungumza Jumapili katika kikao na mjukuu wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) pamoja na msimamizi wa Haram ya Imam Khomeini, Waziri Sadegh aliwasilisha taarifa kuhusu utendaji wa wizara yake katika kipindi hicho, akieleza hatua zilizochukuliwa kurekebisha na kujenga upya nyumba zilizoharibiwa wakati wa mashambulizi.
Alisema mara baada ya kuanza kwa vita hivyo, wizara iliunda kamati maalumu ya kusimamia majanga ili kuhakikisha usafirishaji wa bidhaa muhimu na huduma za usafiri kwa wasafiri unaendelea bila kukwama.
Aidha, Waziri huyo alifafanua kuwa licha ya rada za anga kuharibiwa na Uwanja wa Ndege wa Mehrabad mjini Tehran kushambuliwa mara kadhaa, mamlaka zilifanikiwa kufunga anga ya taifa ndani ya muda usiozidi dakika 45 kama hatua ya dharura. Aliongeza kuwa mzigo mkubwa wa usafiri ulihamishiwa kwenye reli na mtandao wa barabara za nchi, jambo lililosaidia kudumisha huduma muhimu katika kipindi hicho kigumu.
Sadegh alisisitiza kuwa juhudi za kujitolea za wafanyakazi wa wizara na wakandarasi zilichangia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto za vita na kuhakikisha miradi ya maendeleo haikwami.
Your Comment